KILIMANJARO MARATHON KUTIMUA MVUMBI
IJUMAA HUKU WANARIADHA TANZANIA KUJARIBU
BAHATI YAO.
>>Wanariadha kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda wanategemewa kuanza kuwasili mjini Moshi, Kaskazini mwa Tanzania Ijumaa hii kwa ajili ya kushiriki mbio za Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika siku ya Jumapili mapema asubuhi.
Kenya na Uganda ni miongoni mwa nchi zilizopo jirani na Tanzania ambazo wakimbiaji wake maarufu
na wanaochipukia hushiriki katika mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha duniani
(IAAF).
Kuwasili mapema kwa wanariadha hao ambao idadi
yao haijafahamika kwa sababu ni ya wazi (Open) ni kwa ajili ya kusoma njia zitakazotumika na kufanya
usajili katika hoteli ya Keys iliyopo kati kati ya manispaa (municipal) ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mbali na Kenya na Uganda, wanariadha wengine, kwa mujibu wa waandaaji wameanza kuwasili kwa
ajili ya mbio hizo, wengi wao wakiwa watalii kwa ajili ya kupata fursa ya kuuona Mlima Kilimanjaro,
ambao ni mrefu kuliko milima yote barani Africa.
Zaidi ya wakimbiaji 6000 mashuhuri kutoka Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika, Ulaya, America
na Asia wanategemewa kuwania medali za dhahabu, Shaba na Fedha pamoja na pesa taslimu katika
mbio hizo za wazi kwa raia na wageni.
Wanariadha wa Kenya walitawala mbio za mwaka jana ambapo katika mbio ndefu (full marathon- wanaume), nafasi sita za juu zilishikwa na Wakenya
huku David Rutoh-akiwa namba moja na kumaliza mbio kwa muda wa 2:16:06.
Kwa upande wa wanawake (full marathon), Kenya pia ilishinda nafasi nane za juu, mshindi wa kwanza akiwa ni Fridah Lodepa akishinda kwa muda wa 2:40:26 huku Joan Rojich akimaliza wa pili katika muda wa 2:44:24.
No comments: