Recent Posts

MAMBO MUHIMU YALIYO JILI JANA BUNGENI DODOMA DHIDI YA SAKATA LA TEGETA ESCROW.

Wakati hali ikizidi kuwa tete dhidi ya utaifishwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo jana
alipangua hoja zilizotolewa na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), kuhusu ufisadi uliofanyika katika
Akaunti ya Tegeta Escrow na kuacha wananchi njia
panda kwa kutokuelewa nani anasema ukweli kati
yake na kamati hiyo, inayoongozwa na Zitto
Kabwe.

Fahamu kuwa juzi, kamati hiyo ya Zitto iliwasilisha ripoti yake
kuwa imethibitisha kuwa Profesa Muhongo
amekuwa mara kwa mara akilipotosha Bunge na
Taifa kwa ujumla kwamba ndani ya fedha hizo
hakukuwa na fedha za umma ambapo kaamati hiyo ilieleza kuwa imebaini kuwa Profesa
Muhongo ndiye aliyekuwa dalali mkuu
aliyewakutanisha Singh Sethi na James
Rugemalira tena katika ofisi ya umma na pengine
hilo ndilo lilikuwa sababu ya upotoshaji.

Akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu hoja hiyo,
Profesa Muhongo alianza kupangua hoja moja
baada ya nyingine ingawa katika mjadala wa
baadaye, zilihojiwa na wachangiaji wengine
waliohoji uhalali wa vielelezo alivyotoa.

Katika jambo hilo juu ya kutaifisha mitambo
Jana, alieleza kuwa pendekezo la Kamati ya PAC
kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe si sawa kwa
kuwa kulingana na mkataba wa PPA kati ya
Tanesco na IPTL, majukumu ya IPTL yalikuwa ni
kujenga, kumiliki na kuendesha (Build, Own and
Operate – BOO). Hivyo, kutaifisha mtambo huo ni
kukiuka makubaliano katika mkataba wa PPA wa
Mei 26, 1995.

Ukiukwaji wa aina hii ukitokea unaweza kuingiza
Serikali katika mgogoro mkubwa ikiwa ni pamoja
na kushtakiwa kwenye Mahakama za kibiashara
za kimataifa. Aidha, utaifishaji wa miradi ya
uwekezaji binafsi itakuwa ni njia ya kufukuza
wawekezaji.” alisema Muhongo.

Na juu ya gharama za uwekezaji
Kuhusu taarifa ya kamati ya PAC kwamba mwaka
2004 Tanesco ilifungua shauri katika Kituo cha
Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro ya Kiuwekezaji
(ICSID 2) kupinga kiasi kikubwa cha tozo ya
gharama za uwekezaji, Profesa Muhongo alisema
suala hilo si kweli.

Taarifa zaidi ni kuwa alifafanua Tanesco haijawahi kufungua
shauri lolote ICSID ya London au Mahakama
yoyote dhidi ya Benki ya Standard Charterd
kupinga kiasi kikubwa cha Capacity Charge kama
inavyoelezwa na PAC.

“Shauri la ICSID 2 lilifunguliwa Oktoba 31, 2010 na
Standard Chatered Bank Hong Kong (SCBHK) kwa
ajili ya kudai malipo ya deni ililonunua kutokana na
mkopo uliotolewa na mabenki ya ushirika ya
Malaysia kwa IPTL. Wahusika katika shauri hilo la
ICSID 2 ni SCBHK na Tanesco na wala siyo
Tanesco na IPTL." alisema Prof.Muhongo.

Akiongezea zaidi alisema kuwa Februari 12, ICSID ilitoa uamuzi kuhusiana
na shauri la SCBHK na Tanesco na kuwashauri
wakae kukokotoa upya malipo ya Capacity Charge.
Hata hivyo, ilikuwa vigumu kwa pande hizo
kutekeleza uamuzi huo kutokana na pande hizo
kutokuwa na mkataba wa kibiashara baina yao.

“Vilevile, kupitia shauri la madai Na. 60/2014,
lililofunguliwa na IPTL katika Mahakama Kuu ya
Tanzania Aprili 4, ilizuia utekelezaji wa maelekezo
hayo,” alisema.
Uwekezaji wa Sh50,000 kuhusu madai ya PAC
kuwa mtaji wa uwekezaji katika mtambo wa IPTL
ni Sh50,000 na kwamba huo ndiyo ungetumika
kukokotoa gharama za uwekezaji ili kulipa tozo
ndogo kuliko ilivyo sasa, maelezo hayo siyo sahihi.
Alisema ukweli ni kwamba kutokana na uamuzi ya
ICSID 1 ya Julai 12, 2001, gharama za ujenzi wa
mtambo wa Tegeta ni Dola za Marekani 127.2
milioni kama ilivyoelezwa na taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Profesa Muhongo katika taarifa hiyo, pia alisema kuwa
imeelezwa kuwa ilikubalika kuwa uwiano wa deni
na mtaji utakuwa 70:30 ikiwa na maana kwamba,
deni ni Dola za Marekani 89.04 milioni na mtaji ni
Dola za Marekani 38.16 milioni na kwamba uamuzi
huo haujabadilishwa na Mahakama yoyote au mtu
yeyote.

“Tunakubaliana kwamba fedha iliyopokewa kutoka
mabenki ya ushirika ya Malaysia kama mkopo ni
Dola za Marekani 85.86 milioni ambazo kati ya
Dola za Marekani 105 milioni zilizokuwa
zimeidhinishwa,” alisema na kuongeza:
“Swali la kujiuliza je, mtambo huo ulikamilikaje
kwa gharama ya Dola za Marekani 85.86 milioni,
huku gharama halisi ya ujenzi wa mtambo wa
Tegeta ikawa Dola za Marekani 127.2 milioni?
Alisema ni dhahiri kwamba kuna matumizi ya zaidi
ya Dola za Marekani 38.16 milioni ambazo pia
zimetumika kwenye uwekezaji na kwamba Kamati
ya PAC haikuonyesha fedha hizo kuwa sehemu ya
uwekezaji.

PAP na umiliki wa hisa saba
Profesa Muhongo alisema kuwa kwa mujibu wa
taarifa za Brela za Desemba 31, 2013, uhamishaji
wa hisa saba za Mechmar katika IPTL kwenda PAP
ulisajiliwa hapa nchini. Kwa maana hiyo, PAP ni
mmiliki wa asilimia 70 za IPTL. Alisema Kamati ya
PAC imeeleza kuwa PAP siyo mmiliki halali wa hisa
saba za Mechmar katika IPTL lakini kamati
imethibitisha kwamba nyaraka za mauziano kati ya
Mechmer na Piper Link zilipokewa na Harbinder
Singh Sethi ambaye pia ndiye mmiliki wa PAP.

“Kwa uthibitisho huo, kamati inakubali kuwa hisa
za Mechmer katika IPTL zinamilikiwa na PAP,”
alisema Profesa Muhongo.
Akana kuwa dalali
Profesa Muhongo alisema taarifa ya Kamati ya PAC
kwamba yeye ndiye aliyekuwa dalali mkuu
aliyewakutanisha Harbinder Sethi na James
Rugemalira siyo sahihi kuwa tangu Novemba 9,
2011, Rita iliitisha mkutano na kuwakutanisha
wadau wote wa IPTL wakati yeye alikuwa
hajateuliwa kwenye wadhifa huo.
“Mimi kama ni dalali, udalali wangu ni kupeleka
umeme vijijini. Mimi kama ni dalali udalali wangu ni
kusaidia wachimbaji wadogo wa madini na
kupeleka Watanzania kusoma masters (shahada
ya pili) duniani kote.”

Na kitendo cha Serikali kutokuchukua tahadhari
Waziri alisema Kamati ya PAC, imeeleza kuwa
Serikali haikuchukua tahadhari ya kutosha dhidi ya
madai mengine yanayoweza kujitokeza kabla ya
kutolewa kwa fedha kutoka akaunti ya escrow kitu
ambacho alidai si kweli.
Profesa Muhongo alisema kinga iliyochukuliwa
inakidhi matakwa ya kisheria na imezingatia athari
yoyote ambayo ingeweza kutokea baadaye
kutokana na kutolewa kwa fedha katika akaunti ya
escrow.

“Kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali
haikuchukua tahadhari kama ilivyodaiwa na PAC.”
Madai ya Sh321 bilioni
Profesa Muhongo alisema hoja ya PAC kwamba
imejiridhisha kuwa madai ya Tanesco ya Sh321
bilioni yana uhalali japo usahihi wake utapatikana
baada ya kutekelezwa kwa uamuzi wa ICSID 2 na
Tanesco na IPTL kukubaliana kiwango sahihi cha
Capacity Charge haina nguvu.
“Madai ya kwamba Tanesco inaidai IPTL Sh321
bilioni msingi wake ni dhana kwamba mtaji wa IPTL
ni Dola za Marekani 100, sawa na Sh50,000 kwa
wakati huo. Dhana hii ilipuuza ukweli kwamba Dola
za Marekani 38.16 milioni ziliwekezwa kwenye
mradi wa Tegeta,” alisema Profesa Muhongo.

Akimalizia utetezi wake Profesa Muhongo alisema Bodi ya Tanesco
imekana kuyatambua madai hayo ya Sh321
bilioni...
“Kimsingi hata vitabu vya hesabu vya
Tanesco ambavyo vimekuwa vikikaguliwa na CAG,
havionyeshi kuwapo kwa deni hilo.”

MAMBO MUHIMU YALIYO JILI JANA BUNGENI DODOMA DHIDI YA SAKATA LA TEGETA ESCROW. MAMBO MUHIMU YALIYO JILI JANA BUNGENI DODOMA DHIDI YA SAKATA LA TEGETA ESCROW. Reviewed by Unknown on 00:20 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.